TUNDA PAPAI
Tunda papai tamu na lenye ladha ya mvuto.
Papai linastawi katika hali ya hewa ya kitropiki yenye joto kiasi, hali hii muafaka kabisa kwa mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Pwani na mingineyo yenye hali kama hiyo.
Udongo unaofaa kwa papai ni ule wenye rutuba na usiotuamisha maji. Endapo papai litapanwakwenye udongo unaotuamisha maji, mipapai haitadumu itadhurika na maji.
Mipapai ikipandwa na kuwekewa mbolea ya kutosha wastani wa kilo tano mpaka sita za samadi, upo uwezekano ikadumu kwa miaka mitatu ikitoa matunda. Mwaka wa kwanza wa kupandwa mazao huwa si mengi sana, lakini mwaka unaofuata mpapai huzaa sana na kadri miaka inayofuatia mpapa unapoteza uwezo wake wa kuzaa mapapai.
Inashauriwa kutunza mpapa kwa miaka mitatu na hapo kuing'o na kupanda mingine. Mipapai inaweza kupandwa na mazao mengine ambayo hayatauzidi urefu mpapai. Mazao yanayoweza kupandwa na mipapai ni pamoja na nanasi, mahindi nk.
Papai lina soko la uhakika. Papai likiwa shambani laweza kuuzwa kwa shilingi mia tatu 300/= mpaka mia tano 500/=. Hata hivyo papai likitoka shambani na likifikishwa barabarani hasa maeneo ya stendi za magari huko huko vijijini linauzwa siyo chini ya shilingi 1,000/= na likifikishwa mjini ni zaidi ya 1,500/= mpaka 2,000/= na zaidi kutegemea na ubora wake.
Mkulima makini mwenye heka moja aliyepanda mipapai kama 1,000 ana uhakika wa kupata wastani wa shilingi 300,000/= kwa wiki. na kama atakwenda zaidi na kupanda heka tatu basi ana uhakika wa kupata wastani wa shilingi 900,000/= kwa wiki
Mwandishi amefanya utafiti kidogo kwa wakulima wachache, ambao wamesema wanauza mapapai yao kwa walanguzi wadogo wadogo wapitao majumbani mwao kwa baiskeli. Walanguzi hao huwa na matenga makubwa na kununua papai moja kwa shilingi 100/= hadi 200/=. Hii inatokana na ukweli kwamba wanavijiji wengi huwa wamepanda miche michache mashambani mwao, aidha huwa inajiotea kutokana na kula mapapai na kutupa mbegu.
Ni maoni ya mwandishi wa makala hii kwamba hii nayo ni fursa inayoweza kumfanya mwananchi akapambana na maisha yake bila kusubiria ajira za serikali. Ikumbukwe kuwa mwanakijiji huyu pamoja na shughuli hii ya kilimo cha papai; anaweza kuwa na shughuli nyingine kama ya ufugaji wa kuku, mbuzi na ng'ombe wawili watatu wa maziwa.